Waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i amewaonya vikali walimu walio na mazoea ya kutohudhuria vipindi vya masomo shuleni kwa mujibu wa ratiba.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubu kwenye hafla ya kuwazawadi wanafunzi waliotia fora kwenye mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE kule Nyambaria siku ya Jumapili, Matiang'i alisema kuwa shule nyingi nchini huandikisha matokeo duni kutokana na hali ya walimu kukosa kuhudhuria asilimia 90 ya vipindi darasani, hali ambayo amesema itamlazimu kuwachukulia wahusika hatua kali. 

"Kama wizara tumegundua kuwa baadhi ya shule huandikisha matokeo duni kwenye mitihani ya kitaifa kutokana na hali ya walimu kutohudhuria asilimia 90 ya vipindi darasani, na iwapo kuna wanaendelesha tabia hiyo wacha wajue kuwa kamwe hawatavumiliwa," alisema Matiang'i. 

Matiang'i aidha aliwaamrisha wakurugenzi wa elimu kwenye kaunti kuhakikisha walimu wakuu wa shule hawalipishi karo kinyume na viwango vilivyoidhinishwa, huku akiwahimiza wakurugenzi hao kuripoti walimu wanaokiuka viwango vya karo vilivyoidhinishwa ili hatua kuchukuliwa dhidi yao. 

"Kuna lalama tunazozipokea kutoka kwa wazazi kuhusiana na baadhi ya walimu walio na mazoea ya kuitisha viwango vya juu vya karo na ndio sababu nawaagiza walimu wakuu wa shule kuhakikisha kuwa viwango vya karo vinavyolipishwa kwenye shule za umma ni halali," aliongezea Matiang'i.