Huenda walimu wakuu wa shule walio na mazoea ya kuwafurusha wanafunzi shuleni kwa sababu ya pesa za mitihani wakajipata taabani baada ya serikali ya kitaifa kufutilia mbali pesa hizo. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kwenye mahojiano kwa njia ya simu na waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i mapema Ijumaa, Matiang'i alisema kuwa mwalimu yeyote atakayepatikana akiwafurusha wanafunzi shuleni kwa sababu ya pesa za mitihani atachukuliwa hatua za kinidhamu.

"Serikali ya kitaifa ilifutilia mbali pesa za mitihani ya kitaifa kwa wanafunzi wa darasa la nane na kidato cha nne, na wacha iwe onyo kwa walimu wakuu wa shule watakaopatikana wakikiuka agizo hilo," alisema Matiang'i.

Matiang'i aidha aliwaonya vikali walimu walio na mazoea ya kukosa kuhudhuria vipindi vya masomo shuleni akihoji kuwa wataachishwa kazi.

"Kuna walimu walio na mazoea yakukosa kuhudhuria vipindi vya masomo shuleni, hali inayochangia katika kudorora kwa viwango vya elimu nchini na kwa sababu hiyo serikali haitosita kuwaachisha kazi walimu wa aina hiyo," aliongezea Matiang'i. 

Haya yanajiri baada ya Rais Uhuru Kenyatta kurejelea kauli kuwa serikali ilifutilia mbali pesa za mitihani nchini kule Kebirigo alhamisi wiki jana.