Waziri wa elimu Fred Matiang’i amewatahadharisha walimu wakuu nchini dhidi ya kuwasajili wanafunzi wanaoshiriki migomo katika shule zao na kisha kuhamia shule zingine.

Share news tips with us here at Hivisasa

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatatu, Matiang’i alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza visa vya wanafunzi kujiunga na shule zingine baada ya kuharibu mali katika shule zao.

Hata hivyo, waziri huyo alisema walimu wakuu wanakubaliwa kuwasajili wanafunzi kutoka shule zingine ikiwa wanafunzi hao watakuja na barua kutoka kwa wakurugenzi wa elimu katika kaunti ndogo wanakotoka.

Vilevile Matiang’i alionya kuwa serikali haitogharamia hasara yoyote itakayosababishwa na mgomo huo, hivyo sharti wazazi wadhibiti watoto wa ili kuzuia kugharamia uharibifu utakaotokana na wanafunzi kushiriki mgomo.

Aidha waziri huyo amewapa wakurugenzi wa Elimu wa Kaunti makataa ya saa 48 kuandaa ripoti kuhusu tatizo la wanafunzi kuchoma shule.

Mapendekezo ya Matiang’i yanakuja wakati visa vya wanafunzi kugoma vikiripotiwa huku vya hivi punde vikiwa huko Kisii ambapo wanafunzi walichoma mabweni saba baada ya kukatazwa kutazama mashindano ya mataifa ya Ulaya Euro.