Waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i amewaomba walimu walio na nia ya kuwania nyadhifa za kisiasa mwakani kujiuzulu. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu kwenye shule ya upili ya wavulana ya Kisii siku ya Jumatano wakati wa mkutano wa pamoja na walimu wakuu wa shule kutoka eneo hilo, Matiang'i alisema sharti walimu walio na nia ya kuwania nyadhifa za kisiasa wajiuzulu ili kuruhusu tume ya uajiri wa walimu nchini TSC kuanzisha mchakato wa kuajiri walimu wengine. 

"Nina orodha ya walimu walio nia ya kuwania nyadhifa za kisiasa kwenye uchaguzi mkuu ujao, na ni ombi langu kwao kujiuzulu kwa mapema ili kuiruhusu tume ya uajiri wa walimu TSC kuanzisha mchakato wa kuajiri walimu wengine kwa wakati," alisema Matiang'i. 

Matiang'i aidha aliwaonya vikali walimu wakuu wa shule dhidi ya kushikilia nyadhifa za wakurugenzi kwenye kampuni za uzalishaji majani chai akihoji watachukuliwa hatua kali za kisheria. 

"Kuna baadhi ya walimu wakuu wa shule ambao pia wanashikilia nyadhifa za wakurugenzi kwenye kampuni za uzalishaji chai nchini ilhali wana majukumu ya kuziongoza shule na kamwe hilo halitoruhusiwa kwa maana hali hiyo inachanganya elimu pamoja na biashara," aliongezea Matiang'i.