Muungano wa mawakala wa kusajili na kusafirisha wakaazi katika mataifa ya mashariki ya kati, umemtaka Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kuingilia kati na kuifanyia marekebisho sheria iliyobuniwa na Wizara ya Leba nchini kuhusu mawakala hao.
Akizungumza kwenye mkutano wa wananchama wa mawakala hao mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Naibu mwenyekiti wa muungano huo katika eneo la Pwani Mwalimu Mwaguzo alisema kuwa sheria hiyo inawataka mawakala hao kulipa shilingi elfu 500 kwa usajili wa kupata vyeti vya kufanya kazi, pamoja na shilingi milioni tano kama hisa.
Mwaguzo alisema kuwa fedha hizo ni nyingi mno ikilinganishwa na changamoto wanazopitia, licha ya wao kukubali kufanya kazi na serikali.
Mwenyekiti huyo amemwomba Rais Kenyatta kuangazi swala hilo na kuwaondolea gharama hizo.
Aidha, ameitaka serikali kukabiliana vikali na madalali wanaoharibu kazi hiyo kwa manufaa yao binafsi, bila ya kujali maisha ya Wakenya.
"Tunaitaka serikali kusikia kilio chetu na kutuondolea gharama ya kupata leseni za kufanya kazi kwani iko juu sana,” alisema Mwaguzo.
Kilio cha mawakala hao kinajiri siku moja tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta na Waziri wa Maswala ya Kigeni Amina Mohammed na mjumbe kutoka taifa la Saudi Arabia kutia saini mkataba wa kuzuia Wakenya kuhangaishwa nchini humo.