kamati ya bunge kuhusu utekelezaji wa maamuzi ya bunge la kitaifa imesema kuwa mawaziri ambao watakiuka maagizo ya kufika mbele ya kamati hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Akiwahutubia wanahabari katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Jumatano, mwenyekiti wa kamati hiyo Soipan Tuya, alisema kuwa amemtaka Waziri wa Usalama wa ndani Joseph Nkaissery kufika mbele ya kamati hiyo mara kadhaa, lakini bado hajafanya hivyo.
“Waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery anapaswa kufika mbele ya kamati yangu kuelezea kwa nini Wakenya waliofikia umri wa 18 bado hawajapata vitambulisho,” alisema Tuya.
Bi Tuya ambaye pia ni mwakilishi wa kina mama katika Kaunti ya Narok, alisema bunge lilipitisha mswada kuwa kila Mkenya ambaye amefika umri wa miaka 18 anafaa kupata kitambulisho lakini bado swala hilo halijatimizwa.
Aidha, kamati hiyo imesema kuwa inafanya kila juhudi za kisheria kuhakikisha kuwa wananchi wanaruhusiwa kupiga kura wakitumia kadi ya kungojea kitambulisho kama ilivyopitishwa na bunge.