Afisa wa kilimo katika kaunti ndogo ya Subukia, Kenneth Muiruri amesema mavuno ya mahindi katika eneo hilo yanatarajiwa kupungua mwaka huu kufuatia ugongwa wa mahindi wa ‘Maize Lethal Necrosis’.
“Jumla ya ekari 7,000 zimepandwa mahindi ikilinganishwa na ekari 9,000 ambazo kwa kawaida hupandwa mahindi katika kaunti ndogo ya Subukia. Kufikia sasa ingawa ni mapema, hakuna dalili zozote za ugonjwa huo zimeripotiwa,” alisema Muiruri.
Akiongea siku ya Jumanne ofisini mwake, afisa huyo alisema ni jambo la kufurahisha kuona wakulima wameitikia wito na ushauri wa maafisa wa kilimo wa kutopanda mahindi kwa wingi, kwani wengi wamekumbatia kilimo cha vyakula mbali mbali.
“Katika ziara yetu katika mashamba mbali mbali huku Subukia, tulipata wakulima wakishughulikia mimea yao ya maharagwe, viazi, viazi vitamu na ngano,” alisema Muiruri.
Aliongezea: “Tuna tarajia zao la mahindi kupungua. Kilimo biashara ambacho wakulima hawa wamekumbatia kitawapa faida na tunazidi kuwahimiza waendelee na mtindo huu.”
Hata hivyo, afisa huyo aliwataka wakulima waliopanda mahindi kunyunyizia mimea yao madawa ili yasiadhiriwe na ugonjwa huo.
Aliongeza maafisa wa kilimo wako macho katika kuchukua hatua za dharura iwapo dalili zozote zitaripotiwa, na pia wanazidi kutoa uhamasisho kwao jinsi ya kutambua dalili hizo.