Wanakijiji wa Nyamage katika Kaunti ya Kisii walipigwa na butwaa pale ambapo kisa kinachoaminika kuwa cha mazingaombwe ya aina yake kilipotokea mnamo siku ya Alhamisi.
Kulingana na wanakijiji hao, daktari mmoja wa kienyeji alitumia mdomo wake kuwanyonya damu watu walioshukiwa kuwa na uchawi ili kupima kiwango chao.
Daktari huyo kwa jina Dinah Moraa alialikwa na naibu wa chifu wa eneo hilo Sarah Mokua kufuatia visa vingi vya uchawi wa aina hiyo kukithiri kwa siku za hivi karibuni.
“Mimi kama naibu chifu wenu, kutokana na visa vingi vya ‘uchawi wa macho’ vilivyoripotiwa afisini mwangu, nilionelea ni vyema nitafute daktari ili atusaidie kwa sababu tatizo hili linaumiza watoto kwa watu wazima na hata husababisha vifo kama mnavyojua,” alisema Mokua.
Daktari huyo alisema ya kwamba kuna njia nyingi za kupokezwa uchawi huo wa macho hata bila muathirika kujua.
“Mchawi anaweza kukupokeza uchawi huo kwa kukukanyaga katika kidole kikubwa cha mguu, kukutwika au kumtwika kitu kama maji au kuni, anaweza kutia uchawi wake ndani ya maji ya kupika yaliyoinjikwa kwenye jiko na uchawi huo utamwingia kwa damu pale joto lile la maji moto litamuingia atakayepika huku akitokwa na jasho, pia njia nyingine ni ya kubadilishana pesa za sarafu,” aliongeza Mokua.
“Pia wachawi wa aina hii wanaweza kumwagilia nguo zilizoanikwa ama kumwagilia mtu moja kwa moja kwa kumtazama tu kwa macho, yaani kuonana macho kwa macho,” alihoji Daktari huyo.
Daktari huyo wa kienyeji alitumia nyembe kwa kumenya vipaji vya nyuso za watu na kumumunya damu kisha kuitema kwa kartasi nyeupe. Vidudu vingetokezea papo hapo na kujigeuzageuza kwa kartasi hiyo kama mtu huyo ana ule uchawi, na kithibitisha tosha kwamba yeye ni muadhirika, yaani mchawi.
Kati ya watu kadri ya arobaini waliopimwa, sita walipatikana na tatizo hilo, kasha wakaagizwa kununua kondoo mmoja na kuku mwenye anataga ama mwenye ana vifaranga ili wanyama hao watumike kwa matambiko ya kuwasafisha uchawi huo.
“Sasa mmejionea wenyewe, basi itabidi mnunue kondoo na kuku anayetaga ama awe ana vifaranga ili wanyama hao watumike kutambika. Damu yao na ngozi ya kondoo huyo itatumika kuosha uchawi ulio miilini mwenu,” aliagiza Daktari.