Polisi wa eneo la Karai katika eneo bunge la Kikuyu hapo jana walimtia nguvuni mshukiwa mmoja wa ubakaji.
Julius Ndungu, mwenye umri wa miaka 24 alitiwa nguvuni baada ya kutambuliwa na watoto wawili, ambao walidai kuwa alikuwa anawatendea unyama huo.
Watoto hawa walikuwa msichana wa miaka 10 na mvulana wa miaka 11.
Watoto hao walieleza polisi kuwa mwanaume huyo alikuwa amewabaka wakati nyanya yao alikuwa hayupo au ameenda sokoni au shughuli mbalimbali.
Waliongezea kuwa mwanaume huyo alikuwa anawapatia pesa ili wasiseme, huku akiwakemea kwa ukali kuwa watakaposema atawafanyia mabaya zaidi.
Wakazi wa eneo hilo, akiwemo mkazi wa Karai Patrick Kinyanjui alikemea kwa ukali matendo ya mwanaume huyo.
“Kwa nini mwanaume anaharibu maisha ya watoto ilihali kuna kahaba chungu nzima ambao wanaweza msaidia katika mahitaji yake,” alisema Kinyajui.
Nyanya ya watoto hawa alisikitika na kutokwa na machozi aliposikia ni mambo gani yalikuwa yanafanyiwa wajukuu wake.
Mkuu wa polisi eneo la Kikuyu Maweo alidhibitisha tukio hilo, akisema kuwa uchunguzi umeanzishwa dhidi ya uhalifu huo.
Maweo aliongeza kuwa watoto watapelekwa hospitali na hatua za sheria kulingana na matokeo ya uchunguzi zitachukuliwa dhidi ya mhalifu.
Wakazi walionywa dhidi ya kufanya uhalifu, na haswa kwa watoto ambao ni wanyonge na badala yake kulinda watoto na kuona kuwa wanaishi maisha mazuri.
Mshukiwa alizuiliwa katika stesheni ya polisi ya Kikuyu.