Mwanasiasa kutoka Mombasa Ali Mbogo amewahimiza wakaazi wa Mombasa kuwateua viongozi wasomi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mbogo, ambaye ametangaza kuwania kiti cha ubunge Kisauni katika uchaguzi mkuu ujao, amesema kuwa ukosefu wa elimu miongoni mwa viongozi walioko mamlakani umechangia pakubwa eneo hilo kusalia nyuma kimaendeleo.

Akiongea kwenye hafla ya kuhitimu kwa mahafala wa Chuo cha kiufundi cha Kisauni, Mbogo alisema kuwa viongozi ambao hawajasoma hawawezi leta mabadiliko ya manufaa.

Alisema kuwa wakati umefika kwa wakaazi kuwateua viongozi watakao kuza hali ya uchumi ya mwananchi wa kawaida.

Aidha, mwanasiasa huyo amewataka wazazi kuchukua wajibu wa kuwapeleka wanao shuleni.

“Ningependa kuwahimiza wazazi kuzingatia maswala ya elimu, kwani mzazi anapompa muelimisha mwanawe, huwa amempa urathi wa maisha,” alisema Mbogo.

Mbogo alisema kuwa elimu ndiyo suluhu ya janga la ukosefu wa usalama katika eneo la Kisauni, ikizangatiwa kuwa vijana ndio wanaotekeleza uovu eneo hilo.

Vile vile, ameitaka serikali ya kaunti kujenga vyuo vya kiufundi katika kila eneo bunge, kama njia mojawapo ya kuhakisha kuwa vijana wanapata ujuzi mbalimbali utakaowawezesha kujikimu kimaisha.