Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC imehimizwa kulishugulikia kwa kina swala la watu kusajiliwa kama wapiga kura bila ya wao kufahamu.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa, mwakilishi wa wanawake Mishi Mboko alisema kwamba visa vya watu kujipata wamesajiliwa bila kufahamu vimeongezeka, na kuitaka IEBC kutatua swala hilo haraka.
Mboko alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona visa hivyo vikiendelea kuripotiwa pasi hatua zozote kuchukuliwa.
Mwakilishi huyo wa wanawake alisema kuwa hali hiyo inawachanganya wananchi na kupelekea wengi wao kukosa kusajiliwa.
Aidha, ameitaka IEBC kuongeza mashine za kusajili wapiga kura, kwa kuwa idadi ya watu ambao bado hawajasajiliwa ingali ni kubwa.
Vile vile, ameitaka tume hiyo kuzidisha hamasa miongoni mwa wananchi kuhusiana na zoezi la kuwasajili wapiga kura linaloendelea kote nchini.
Mboko aidha ameahamiza wakaazi wa Mombasa kutopuuza zoezi hilo na badala yake kujitokeza kwa wingi.