Hisia mseto zimeanza kuibuka miongoni mwa viongozi wa mrengo wa Cord kutokana na hatua ya kuwasilishwa mapendekezo ya kujadiliwa upya sheria ya uchaguzi nchini.
Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko ameikosoa hatua hiyo kwa kusema kuwa inakiuka maafikiano yaliyotekelezwa na pande zote mbili za mirengo ya kisiasa, wakati wa mchakato kuhusiana na mageuzi ya sheria hiyo ya uchaguzi.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Bi Mishi alidokeza kuwa hamna haja ya kufanya mjadala wa kubadili sheria hiyo ya usimamizi wa uchaguzi ilhali uwakilishi wa pande zote mbili uliafikiana.
Kiongozi huyo alisema kuwa hatua ya kuifanyia sheria hiyo mageuzi huenda ikafanya wananchi wakapoteza imani kuhusiana na kuandaliwa kwa uchaguzi huru na wa haki.
“Ikiwa pande zote mbili zilikubaliana wakati wa awali, hamna haja ya kufanyia sheria hiyo marekebisho kwani itatoa Wakenya imani na usimamizi wa uchaguzi mkuu ujao,” alisema Bi Mishi.
Kauli ya Mboko inajiri huku wabunge wakitarajiwa kukutana hapo kesho kujadili uwezekano wa kuifanyia marekebisho sheria hiyo.