Mwakilishi wa wanawake kaunti ya Mombasa Mishi Mboko amewataka viongozi serikalini na vitengo husika kuheshimu katiba na kuwapa wanawake thuluthi moja kwenye uteuzi wa kazi.
Hii ni kwa mujibu wa katiba ya Kenya.
Mwakilishi huyo aliwapa changamoto wanawake kupigania haki zao ili wapate mgao wa nafasi za serikali na kuacha kukaa kungojea kazi kuwatafuta. Alisema kuwa nyakati za wanawake kubaguliwa kwa sababu ya kuwa na kisomo kidogo haupo tena hivyo basi akawasihi wakazi wa kaunti hiyo kuwasomesha wanao ili wapate nafasi za kazi zinapochipuka.
Mboko alikuwa akisema haya mjini Mombasa siku ya Jumatano, ambapo alishtumu mwelekeo ambao ulifuatwa baada ya kuondolewa kazini aliyekuwa naibu wa inspekta mkuu wa polisi Grace Kaindi. Nafasi yake ilijazwa na mwanamume hali ambayo alisema ni kinyume na katiba.
“Sharti katiba ifuatwe na theluthi moja itengewe wanawake kwenye idara za serikali,” alisema Mboko.
Alimtaka waziri wa usalama wa nchi Joseph Nkaiserry kuangazia suala hilo badala ya kusema kuwa hamna wanawake ambao wana viwango vya ujuzi.
Aidha, aliwataka wawakilishi wa kike pamoja na viongozi wengine wa kike na wale wa kisiasa kwa mkumbo kuhakikisha kuwa katiba mpya inafuatwa na kutekelezwa vilivyo.