Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko ametofautiana na kauli ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho ya kutaka wanafunzi wa chuo kikuu cha Mombasa kutopata usadizi wa karo baada ya kuchoma magari ya kaunti.

Mboko alisema siku ya Alhamisi kwenye hafla ya kufuzu kwa mahafala wa chuo hicho kuwa wanafunzi wa chuo hicho wataendelea kupata usaidizi wa karo, kinyume na taarifa zilizotolewa na serikali ya kaunti kwamba watachukua hatua za kinidhamu kwa wanafunzi wa chuo hicho kwa kuchoma gari la serikali hiyo.

Mwakilishi huyo aliongeza kuwa ni jukumu na haki kwa kila mwanafunzi katika kaunti ya Mombasa kupata usaidizi wa kifedha kulingana na katiba.

Aidha, Mboko aliwasihi wanafunzi hao kuzingatia masomo na kutojihusisha na visa vya utovu wa nidhamu ili kukuza viwango vya elimu jijini.

Itakumbukwa wanafunzi wa chuo hicho wanadaiwa kuchoma magari ya serikali ya kaunti mwezi mmoja uliopita baada ya kushiriki mgomo.