Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Bi Mishi Mboko ameelezea masikitiko yake kwamba wanawake wengi mjini humo hawajajitokeza wazi na kuwania nasafi za uongozi.
Bi Mboko alisema kuwa wanawake wa eneo hilo wanaogopa kujitosa katika maswala ya siasa na uongozi, na kuongeza kwamba hali hiyo huenda ikawafanya wanawake kuendelea kudharauliwa katika jamii.
Akiongea siku ya Jumanne katika uwanja wa Tononoka mjini humo wakati wa hafla ya kusherehekea siku ya wanawake ulimwenguni, Mboko alisisitiza kwamba wanawake wanaweza kuongoza huku akitoa mfano wa yeye mwenyewe.
“Hapo mwanzo ilikuwa ni changamoto lakini sasa tunaona wanawake wametosha kuongoza kwani wamehamasishwa vya kutosha na ndio maana tunawaomba wajitokeze na kuwania nyadhifa za uongozi,” alisema Mboko
Mwakilishi huyo aliongeza kuwa anasikitishwa kwa kuwa idadi ya wabunge wa kike katika Kaunti ya Mombasa ni ndogo mno ikilinganishwa na wanaume.
Mboko alisema kuwa wanawake wengi wamekuwa na dhana kwamba nafasi yao ni ya uteuzi pekee badala ya kujitokeza kusimama wima na kuomba kura kwa wananchi.
“Wamama wako na raslimali zote zinazohitajika kwa hivyo tusingoje tu viti vya kuteuliwa kwa sababu hata hii leo hapa tunaongelea kuhusu usawa wa kijinsia,” alisema Mboko.
Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Kilifi Bi Isha Jumwa aliyehudhuria hafla hiyo aliwapongeza akina mama waliojitokeza kwa sherehe hiyo akisema kwamba hiyo inaonyesha kwamba wameanza kufahamu haki zao.