Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko amewashutumu wanajeshi katika kambi ya Mtongwe, kwa madai ya kuwanyanyasa wakaazi wa Likoni nyakati za usiku.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza katika uwanja wa Tononoka wakati wa maadhimisho ya siku ya Jamhuri, Mboko alisema kuwa wanajeshi hao wanakiuka katiba kwa kuwachapa wakaazi hasa wanapoelekea katika maombi ya usiku.

“Vijana, wazee na wanawake katika eneo la Likoni hawana amani kabisa kwani wanachapwa kila siku wanapoelekea katika maombi ya usiku,” alisema Mboko.

Mboko ametaka wanajeshi wanaojihusisha na visa hivyo kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Aidha, Mboko alidai kuwa wanajeshi hao wanahusika katika mauaji ya kiholela katika eneo hilo.

Hata hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki alipuzilia mbali madai hayo na kusema kuwa wanajeshi hao kamwe hawajahusika katika visa hivyo.

“Wanajeshi wetu hawajatekeleza oparesheni yoyote katika eneo la Likoni na Mombasa kwa jumla, hizo ni porojo zisizokuwa na msingi,” alisema Achoki.

Alisema kuwa kwa sasa maafisa wa polisi katika eneo hilo wana uwezo wa kudhibiti usalama pasi msaada kutoka kwa wanajeshi.