Mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Mombasa amesema sheria ya thuluthi mbili ya jinsia katika maswala ya uongozi kamwe haipaswi kupingwa na wanaume wala viongozi humu nchini.
Akiwahutubia wakazi mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Bi Mishi Mboko alisema kuwa sheria hiyo hailengi kuinua hali ya wanawake katika uongozi bali jinsia zote mbili.
Mboko alisema kuwa wanaume wanaopiga vita kupitishwa kwa sheria hiyo bungeni wanamalengo yao binafsi ya kisiasa ambayo huenda yakadunisha hadhi ya mwanawake katika maswala ya uongozi.
“Tuko na mswada ambao unazungumzia mambo ya thuluthi mbili na lazima watu wafahamu kwamba ni jambo ambalo liko katika katiba na katiba ni sheria ya mama. Sheria inasema kusiwe na asilimia zaidi ya thuluthi mbili ambayo ni jinsia moja hivyo basi sio jambo la akina mama pekee,” alisema Mboko.
Kiongozi huyo ameshikilia kupigania haki ya akina mama katika maswala ya uongozi bungeni kwa kuwashirikisha viongozi wanawake wa kisiasa ili kuhakikisha sheria hiyo itapitishwa na kuwa sheria kwani maswala ya uongozi humu nchini yameegemea upande moja.
“Ni vile tu wabunge akina mama ni wachache lakini kesho itakuwa wabunge wa kiume ni wachache. Hivyo basi, sheria hiyo itawasaidia kwani watakuwa wanapitia changamoto kama hizi,” alisema Mboko.
Mboko alisema sheria hiyo ni muhimu mno kwani itawawezesha wanaoishi na ulemavu na makundi mengine yaliyo na mahitaji maalum kuingia uongozini na kutetea maslahi ya wale waliyotengwa katika Jamii.
Mboko ametaka sheria hiyo itekelezwe kikamilifu ili Kenya ifikie mataifa mengine ya Afrika Mashariki ambayo yameimarika kutokana na kujumuishwa kikamilifu kwa wanawake katika maswala ya uongozi, maamuzi ya kidemokarsia na maendeleo kwa jumla.
“Nchi kama ya Rwanda ilikuwa na vita vya kikabila lakini sasa hivi akina mama wako asilimia 64 upande wa jinsia. Taifa la Tanzania na Uganda wako asilimia 35 na 36 lakini sisi tuko asilimia 19 ambapo sisi katika kiuchumi tumebobea kuliko nchi hizi nyingine,” alisema Mboko.
Tayari mswada kuhusiana na swala hilo la thuluthi mbili ya jinsia katika maswala ya uongozi umewasilishwa bungeni na kuzua malumbano miongoni mwa wabunge wanawake na wale wanaume huku kila upande ukionekana kuvutia kwake.