Gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua amewakemea baadhi ya wabunge ambao wanasemekana kumpiga kisiasa katika kaunti hiyo huku wakilenga kuangusha serikali yake chini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mbugua ambaye alikuwa akizungumza jijini Nakuru siku ya Jumatano amedokeza kuwa wabunge hao ambao hakuwataja wanafanya kila wawezalo ili kulemaza shughuli zake za kutumika wananchi wa eneo hilo badala ya kuungana naye katika kuendeleza eneo hilo.

"Kunao baadhi ya wabunge ambao hawalali huku wakiwa na nia ya kusitisha miradi ambayo tunatoa kwa wananchi. Kazi yao ni kuzua rabsha na kutenganisha watu badala ya kutumikia wananchi katika eneo bunge lao," Mbugua alisema.

Mbugua alitaja kisa cha kuzomewa na baadhi ya vijana wakati wa ziara ya rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto katika eneo hilo mapema mwezi huu kama mfano bora wa jitihada za wapinzani wake kumwangamiza.

‘Visa vya hivi karibuni ni wazi kuwa wabunge hawa wana nia za kibinafsi ila si kuleta maendeleo. Baadhi wao wamekataa kuuungana na serikali yangu na kuchukua mkondo tofauti.’ Mbugua aliongezea.

Gavana huyo pia amewahakikishia wananchi wa eneo hilo kuwa atazidi kutimiza ahadi zake licha ya pingamizi hizo na kuwaomba viongozi wanaompinga kuungana naye kuimarisha eneo hilo.

Picha: Gavana wa Nakuru Kinuthia Mbugua katika hafla ya hapo awali. (Maktaba)