Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua ameshtumu vikali viongozi wanaotoa matamshi ya chuki ambayo huenda yakazua vurugu akisema hatavumilia tabia hiyo.
Gavana mbugua pia alionyesha kughadhabishwa kwake na mazoea ya baadhi ya viongozi kutoka maeneo mengine kuandaa mikutano mjini Nakuru.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika eneo la Karagita, mjini Naivasha wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani, Gavana Mbugua alisema kwamba viongozi hao wana maeneo wanayoongoza na kutokana na hilo, wanaweza kuyatumia maeneo hayo kujadili maswala hayo.
“Siwezi kuwaruhusu viongozi kama hao kuja kwenye Kaunti ya Nakuru kuvuruga amani huku wakituwacha kwenye shida wanaporejea kwenye kaunti zao,” alisema Mbugua.
Aliongezea, “Kaunti hii ina makabila mengi yanayoishi kwa amani na umoja. Kwa nini wasifanye mikutano hiyo kwenye maeneo yao?”
Wakati huo huo, Gavana Mbugua alisema kwamba atahimiza kampuni zilizo mjini Naivasha kama vile zile za maua, ziwape vijana wa eneno hilo ajira ikizingatiwa kuwa ukosefu wa kazi ni chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama miogoni mwa wakazi wa eneo hilo.
“Wakati umewadia kwa kampuni hizi kuwapa watu wetu kazi. Kuna nafasi nyingi za kazi katika eneo hili kutokana na nafasi nyingi za uwekezaji katika sekta ya maua na kawi. Tutahimiza kampuni hizi kutoa ajira,” alisema Mbugua.
Aliongezea kwamba ujenzi wa reli mpya ya SGR utakaoendelezwa hadi mjini Naivasha utapelekea nafasi zaidi za ajira kubuniwa.
“Serikali ya kitaifa imekubali kuendeleza ujenzi wa reli mpya ya kisasa ya SGR hadi kwenye kaunti ya Nakuru. Hatua hii itawapa maelfu wa watu kazi katika eneo hili na nina uhakika katika siku za usoni, ukosefu wa ajira utazikwa katika kaburi la sahau,” alisema Mbugua.
Siku ya kimataifa ya Amani iliadhimishwa huku mamia ya vijana na wanawake kutoka maeneo mbalimbali ya Naivasha wakishiriki katika mechi ya kandanda.