Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua amewaonya wakazi kuwa kuwa watachukuliwa hatua za kisheria iwapo watapatikana wakiendeleza biashara ya pombe haramu.

Akizungumza siku ya Alhamisi katika wadi ya Kabatini alipozindua miradi mbalimbali ya maji, Mbugua alisema serikali yake haitachoka kuendeleza vita dhidi ya pombe haramu.

“Ni jambo la kusikitisha kuona wananchi wanaendelea kutumia pombe haramu. Kama serikali, tutazidi kufuatilia watu hawa ambao wanaendelea kutengeneza na kutumia pombe hizo maanake ni jukumu letu kuhakikisha afya bora kwa kila mmoja,” alisema Mbugua.

Mbugua pia aliwaomba wananchi kusaidiana na serikali kuwatambua watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ili hatua dhabiti ichukuliwe dhidi yao.

“Inahitaji sote tuungane ili kuangamiza pombe haramu. Ndiyo maana nawaomba wananchi, ikiwa wewe ni mzee, kijana au kiongozi yeyote yule kusaidiana na polisi katika vita hivi kwa kuripoti wanaoaminika kuendeleza biashara hii,” alisema Mbugua.

Gavana huyo pia alisikitishwa na visa vya baadhi ya vijana kujihusisha na pombe haramu na kusahau kuzingatia masomo yao, huku akiwaomba wazazi wawe macho na kuwachunga watoto wao.