Kamati ya seneti kuhusiana na uhasibu wa pesa za umma itamhoji Gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua kuhusiana na utumizi wa fedha katika kaunti.
Seneta Mteule katika kaunti ya Nakuru Martha Wangare ambaye ni mwanachama wa kamati hiyo amesema katika awamu ya kwanza ambayo walimpiga msasa Gavana Kinuthia, hakubainisha wazi jinsi ambavyo fedha zilizotolewa na serikali ya kitaifa zilizvyotumiwa na Kaunti ya Nakuru.
Akizungumza kwenye sherehe za siku ya mashujaa siku ya Jumanne katika eneno la Gitare mjini Gilgil, Wangare alisema kwamba ni jambo la kutia wasiwasi kuona kuwa ni Sh800,000 pekee zilizotumiwa kufanya maendeleo kati ya shilingi bilioni tano zilizotengewa kaunti.
“Tumekuwa tukichambua akaunti za kaunti ya Nakuru. Kati ya zaidi ya shilingi bilioni saba ambazo zilikuja Nakuru, sio zaidi ya bilioni moja ambazo zimetengewa maendeleo Nakuru. Ni milioni mia nane ndio imeenda kwa miradi ya maendeleo. Kuna mambo ambayo lazima tuangalie kama tunataka kusema ugatuzi umefanikiwa,” alisema seneta huyo.
Pamoja na hayo, seneta wangare ameashiria kwamba gavana wa kaunti ya nakuru kinuthia mbugua aliwarifu kuwa kiwango kidogo cha fedha kilitengewa maendeleo kutokana na gharama kubwa ya matumizi ya serikali ya kaunti ya Nakuru.
Kulingana naye, tayari wamemjuza Gavana Kinuthia Mbugua kuwa wanahitaji orodha iliyo wazi inayoonyesha watu waliolipwa na kiwango kipi cha fedha walicholipwa katika awamu ya pili ya kumpiga msasa.
“Tumetoka kuangalia njia ya kugawa fedha kwenye kaunti ya Nakuru wiki iliyopita na sisi kama watu wa Nakuru tukaikataa. Tutarudi kukutana tena ndio tujadiliane kwa sababu tunataka pesa zaidi kwa sababu hii kaunti ina watu wengi. Hatutaki tunywe chai bila maziwa na kuna maziwa ambayo tungetumia kunywa chai nzuri. Ni sharti uwajibikaji wa pesa uwe,” alisema Wangari.
Akizungumza kuhusiana na jinsi kaunti zinavyotumia fedha, Wangare alihimiza umma kuwa macho na kutaka kujua zaidi kuhusiana na miradi ambayo imefadhiliwa na serikali za kaunti.
Aidha, ameweka bayana kuwa ni muhimu kwa serikali zote za kaunti kuhakikisha kuwa asilimia 30 ya fedha wanazotengewa kutoka kwa serikali ya kitiafa inatumika kwa miradi ya maendeleo.
Wangari alisema seneti itaendelea kuchunguza jinsi serikali za kaunti zinzvyotumia fedha na kutokana na hilo, magavana wanafaa kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kwa njia inayostahili.