Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua amesema kuwa taasisi tajika zina wajibu muhimu wa kudumisha amani katika serikali yoyote ile.
Mbugua alisema watu hutegemea taasisi kama vile mahakama na tume za uchaguzi kupata suluhu na endapo zitakosa kutoa mwelekeao mwafaka, huenda hali ya amani ikawa ya msukosuko.
Akizungumza afisini mwaka alipokaribisha ujumbe kutoka nchini Zimbambwe na Malawi ulio na wajibu wa kuangalia hali ya amani na mapatano nchini siku ya Alhamisi, Gavana Mbugua alisema kuwa uwepo wa kitengo cha kudhibiti hali au matamshi ni muhimu katika kuhakikisha kuna amani.
“Matamshi ya chuki kwa mfano katika katiba yetu yamedhibitiwa kama njia ya kuhakikisha matamshi hayo yanayoweza kuvuruga amani hayatolewi. Ni muhimu kwa mataifa mengine kuzigatia hilo ili kudumisha amani,” alisema Mbugua.
Aidha, alisema kuwa udhibiti wa mitadao ya kijamii ni jambo kuu linalofaa kuzingatiwa katika maswala ya amani.
Gavana pia alisema suluhu zilizopatikana hapo awali kwa tatizo fulani zinaweza kutumika tena lakini matokeo huenda yakawa tofauti.
“Mfano mzuri kwetu ni kubuniwa kwa serikali ya muungano mwaka wa 2008 ambayo kwa wakati huo ilikuwa suluhu la kurejesha amani. Hata hivyo, suluhu hiyo haikufanikiwa pakubwa katika upande wa kuwahudumia wakenya,” alisema Mbugua.