Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir ameikosoa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini IEBC kwa kutoangazia swala la kampeni ya Okoa Kenya.
Nassir alidai kuwa jinsi IEBC ilivyolitatua swala hilo inaonyesha wazi kuwa inaegemea upande wa mrengo wa Jubilee, kuongeza kuwa kutupiliwa mbali kwa shinikizo lao ni wazi kuwa taifa hili haliangazii demokrasia.
Akizungumza katika eneo bunge lake la Mvita siku ya Jumamosi, Nassir alisema kuwa kama viongozi wa mrengo wa Cord, watahakikisha kuwa wanapigania haki za Wakenya licha ya swala lao la kutaka kubadilisha katiba ya nchini kupitia shinikizo lao la kura ya maoni kugonga mwamba.
Mbunge huyo aliwataka Wakenya kuzidi kuunga mkono shinikizo za mrengo wa Cord kwa kusema kuwa mrengo huo ndio unaoweza kubadilisha uongozi duni unaoendelezwa na serikali ya Jubilee.
Alisema kuwa Wakenya ndio wenye uwezo wa kubadili uongozi wa taifa hili kwa kuwachagua viongozi bora na waadilifu kama Kinara wa Cord Raila Odinga.
“Tumegundua kuwa IEBC inaegemea upande wa serikali ya Jubilee na sisi kama Cord hatuwezi tukaitambua kama tume inayoweza kusimamia uchaguzi mkuu kwa sababu itatangaza Jubilee ndio washindi na sisi tunajua tutawashinda,” alisema Abdulswamad.
Kauli ya mbunge huyo iliungwa mkono na Spika wa bunge la Kaunti ya Mombasa Thadius Rajwayi aliyesema kuwa watahakikisha wanawashinikiza Wakenya kuunga mkono Cord katika uchaguzi mkuu ujao.