Mbunge wa eneo la Borabu Ben Momanyi amekabidhi shule ya upili ya Omonayo iliyoko eneo bunge lake shilingi nusu milioni kutumika kusajili wanafunzi kufanya mtihani wa kitaifa kwa mara nyingine baada ya matokeo ya wanafunzi hao wa mwaka jana kufutiliwa mbali.
Matokeo ya wanafunzi wa shule hiyo yalifutiliwa mbali kwa kudaiwa kuhusika kwa visa vya udanganyifu haswa somo la Chemia.
Akizungumza siku ya Jumanne katika shule hiyo, Momanyi alisema ni jambo la kuhuzunisha wakati wanafunzi wanasoma hadi kidato cha nne na kukosa matokeo yao baada ya kutia motisha shuleni.
Momanyi alisema pesa hizo zitatumika kuwasajili wanafunzi hao wote wa mwaka jana ili warudie mitihani huo, huku akisema pesa zitakasosalia zitumike kufanyia shule hiyo ujenzi.
“Naomba wanafunzi wote kutia motisha katika masomo maana masomo ni msingi wa maisha katika ulimwengui huu tunakoishi,” alisema Momanyi.
“Tume ya mitihani nchini KNEC ilifanya vibaya kufutilia mbali matokeo ya mitihani katika shule hii maana hiyo ni njia moja ya kufanya wanafunzi kupoteza imani na tume hiyo na kuogopa masomo maana hawapati kile wanatarajia kukipata,” aliongeza Momanyi.
Momanyi aliahidi kuhakikisha viwango vya masomo vinainuka zaidi katika eneo bunge lake la Borabu kaunti ya Nyamira.
Picha: Mbunge Ben Momanyi (kulia) katika hafla ya awali. Amekabidhi shule ya upili ya Omonayo nusu milioni kutumika kusajili wanafunzi kufanya mtihani wa kitaifa baada ya matokeo ya wanafunzi hao wa mwaka jana kufutiliwa mbali. Star/the-star.co.ke.