Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba amekanusha madai ya kufadhili makundi haramu.
Mbunge huyo aidha ametishia kumshtaki mtu yeyote atakayemhusisha na makundi hayo.
Haya yanajiri baada ya mfanyabiashara maarufu kutoka Mombasa, Ali Mbogo, kumshtumu Bedzemba siku ya Jumatatu kwa madai ya kuyapa makundi hayo ya kigaidi fedha.
Mbogo alisema kuwa alishambuliwa na vijana waliokuwa wamejihami kwa visu alipokuwa ametoka kuhudhuria hafla ya mazishi.
"Tangu wakaazi na maafisa wa usalama kuanza kulalamikia swala hili, mbunge huyo hajakashifu magenge hayo kama inanvyostahili. Hii inaonyesha wazi yeye anawafahamu,” alisema Bw Mbogo.
Hapo awali, mshirikishi wa usalama katika kanda ya Pwani Nelson Marwa alisema kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wanaofadhili makundi haramu.
Hata hivyo, Bedzimba alisema kuwa hana uhusiano wowote na makundi hayo.
"Nitamshtaki mtu yeyote atakayenihusisha na makundi hayo ili waweze kufika mahakamani kuthibitisha madai yao. Kama kiongozi, nia yangu ni kuwatumikia watu wangu. Mimi namheshimu Marwa kama afisa wa usalama lakini anapaswa kuzingatia kupambana na uhalifu,” alisema Bedzimba.