Mbunge wa Mvita Abduswamad Nassir, amekanusha madai kuwa uongozi wake katika eneo bunge hilo umechangia ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, kwa kukosa kutenga mahala pa kurekebisha tabia kwa waathiriwa wa mihadarati.
Akiongea baada ya kutembelea Hospitali ya Majengo siku ya Alhamisi, mbunge huyo alisema kuwa kuna waathiriwa wengi wa mihadarati ambao wamepewa msaada na kurudia hali zao za kawaida.
“Nimejaribu kadri ya uwezo wangu kushirikiana na Idara za Usalama haswa maafisa wa polisi kuhakikisha kuwa walanguzi wa mihadarati katika eneo hili wamekamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Nassir.
Hapo awali, Mohamed Tenge ambaye ni mpinzani wa Nassir alikuwa amedai kuwa uongozi wa mbunge huyo hautilii maanani umuhimu wa kurekebisha tabia ya vijana walioathirika na mihadarati.