Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi akiwahutubia wanahabari katika hafla ya awali. [Photo/ standardmedia.co.ke]
Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi amelaani hatua ya maafisa wa polisi kumtia mbaroni mwakilishi wa wadi ya Airport Ibrahim Omondi.
Omondi alitiwa mbaroni usiku wa kuamkia Ijumaa akiwa nyumbani kwake.
Akizungumza nje ya kituo cha polisi cha Bandari siku ya Ijumaa, Mwinyi aliitaja hatua hiyo kama ya kukandamiza haki na uhuru wa mwakilishi huyo, ikizingatiwa anatoka mrengo wa NASA.
“Huu ni ukandamizaji wa uhuru na haki za viongozi hasaa wa NASA,” alisema Omar.
Mwinyi aliitaja hatua hiyo kama njama ya serikali kuwakandamiza viongozi wa NASA kutoka Kaunti ya Mombasa.
“Kwa muda sasa serikali inakandamiza viongozi wa NASA kote nchini pasi sababu za maana,” alisema Omar.
Familia ya Omondi ikiongozwa na Kenneth Evance imelaani kitendo hicho kwa kusema haki na uhuru wa kiongozi huyo imekiukwa.
Evance alisema kufikia siku ya Ijumaa bado hawakuwa wamemuona ndugu yao baada ya kutiwa mbaroni.