Mbunge wa Jomvu amejitokeza kuwatetea maafisa wa trafiki walioachishwa kazi baada ya kukataa kupigwa msasa katika zoezi lililoandaliwa na Tume ya huduma kwa polisi NPSC.
Akiongea siku ya Jumatatu katika eneo bunge la Jomvu kwenye hafla iliyowaleta pamoja maafisa wa polisi, Badi Twalib aliitaka Tume ya NPSC kutowafuta kazi maafisa hao na badala yake kuwapa nafasi ya kujitetea kama raia wa kawaida dhidi ya madai hayo ya ulaji hongo.
"Ipo haja kubwa sana ya kufuata sheria inavyotakiwa. Badala ya kupigwa kalamu pasipo kusikizwa, maafisa hao wangepaswa kupewa nafasi ya kujitetea kwani polisi sio adui yetu,” alisema mbunge huyo.
Tume hiyo inayoongozwa na Johnston Kavuludi tayari imewaachisha kazi maafisa 302 wa trafiki baada ya kukataa kuhojiwa.