Mbunge wa Nyali Hezron Awiti ameilaumu serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa kuharibu sanamu ililochongwa kwa muundo wa mamba, iliyokuwa nje ya shamba la Mamba village.
Mbunge huyo alikashifu hatua hiyo na kudai kuwa huenda ilichangiwa na sababu za kisiasa.
Akizungumza baada ya kuzuru eneo hilo siku ya Alhamisi, Bwana Awiti alisema kuwa hana pingamizi na serikali ya kaunti kutaka kufanya upanuzi wa barabara, ila wangemuarifu mapema ili kumpa nafasi ya kuondoa sanamu hiyo bila kuiharibu.
Sanamu hiyo ambayo iliundwa miaka 41 iliyopita, ilikuwa kivutio kuu kwa watalii ambao walikuwa na mazoea ya kupiga picha kando ya mamba huyo aliyechongwa na wataalam kutoka nchi ya Israeli.
Hata hivyo, Bwana Awiti amesema kuwa atawatafuta wataalam ili waweze kutengeneza sanamu nyingine inayofanana na hiyo.