Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Uchaguzi wa viongozi wa Muungano wa Wabunge wa Pwani unaendelea kupokea shutma kutoka kwa viongozi mbalimbli kutoka eneo hilo.

Uchaguzi huo uliofanyika siku kadhaa zilizopita ulishuhudia aliyekuwa mwenyekiti, Gideon Mung’aro, kuondolewa kwenye wadhfa wake, jambo linalotajwa kama mbinu ya kisiasa.

Mbunge wa Garsen Kaunti ya Tana River Ibrahim Sane, alisema bado anamtambua Mung’aro kama mwenyekiti wa muungano huo hata baada ya kuondolewa kwenye wadhfa wake.

Kiongozi huyo alisema kwamba wabunge wengi kutoka eneo hilo hawakuhusishwa kwenye uchaguzi huo, na kuongeza kuwa jambo hilo linazua maswali miongozi mwao.

Akiongea siku ya Jumatatu katika eneo bunge lake, Sane alidokeza kwamba takriban wabunge 24 hawakuwepo wakati wa uchaguzi huo na kutaja hatua hiyo kama mbinu ya kisiasa iliyotumika kuficha ukweli.

Nafasi ya Mung’aro kama mwenyekiti wa muungano huo ilichukuliwa na mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga.

Kumekuwa na maswali mengi miongoni mwa viongozi kutoka eneo hilo, baada ya kubainika kuwa wote waliochaguliwa wanatoka mrengo wa upinzani Cord.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideo Mung’aro na mwenzake wa Lungalunga Khatib Mwashetani walitemwa nje ya muungano huo huku baadhi ya viongozi wakitaja hatua hiyo kama adhabu baada ya wao kuonekana wakiunga mkono upande wa Jubilee.