Serikali ya kitaifa imehimizwa kuruhusu matokeo ya mitihani ambayo iliyotupiliwa mbali ya kidato cha nne mwaka jana kusahihishwa upya ili wanafunzi waliokosa matokeo yao kupata haki kupitia majibu yao mapya.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa idadi kubwa ya wanafunzi waliokosa matokeo yao huenda ndoto zao zikaambulia patupu katika maisha yao ya usoni.
Kulingana na mbunge wa eneo bunge la Nyaribari Chache kaunti ya Kisii Richard Tong’i, si jambo nzuri wakati wanafunzi 5,100 wanakosa matokeo yao ya mitihani na kuomba serikali kuruhusu mitihani yao kusahihishwa upya ili kuwapa haki.
“Ndoto za wanafunzi 5,100 zinaonekana kuzimwa kufuatia kukosa matokeo yao ya mitihani hapa nchini," alisema Tong'i.
"Naomba serikali kuruhusu mitihani yao kusahihishwa upya maana bodi mpya ya tume ya KNEC imechaguliwa ili wanafunzi wapate haki zao,” aliongeza Tong’i.
Wakati huo huo, Tong’i alisema ni vyema kuwa serikali ilivunjilia mbali tume ya zamani ya KNEC na kusema huenda wanafunzi wakapata haki zao katika siku za usoni .