Wazazi, walimu pamoja na kamati za shule katika eneo bunge la Mvita wametakiwa kuunga mkono mchakato wa kuunganishwa kwa shule ili kuboresha usimamizi wa raslimali zitakazofaidi shule hizo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Alhamisi na bodi za usimamizi wa shule za msingi zilizoko eneo bunge hilo, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharif Nassir alisema kuwa tayari amewasilisha ombi hilo kwa bodi ya elimu ya Kaunti ya Mombasa na wanasubiri matokeo.

“Tayari nimeshawasilisha pendekezo hilo na tunasubiri matokeo kutoka kwa bodi ya elimu katika Kaunti ya Mombasa ili tuweze kuokoa raslimali,” alisema Nassir.

Aidha, alisema kuwa shule zilizoko eneo hilo ni nyingi huku zingine zikiwa kubwa lakini zimekosa wanafunzi, huku zingine zikiwa na nafasi ndogo, hivyo kuunganishwa kutafaidi shule hizo kwa kiwango kikubwa.

Miongoni mwa shule alizosema wananuia kuunganisha ni ile ya Ziwani na Bahari, Ronald Ngala na Burhania pamoja na Mary Cliff.

Nassir alisema kuwa kuna baadhi ya madarasa yanayosalia matupu kutokana na uhaba wa wanafunzi.

Wakati huo huo alisema kuwa kupitia kwa hazina ya ustawishaji wa eneo bunge mwaka huu, wametenga fedha zitakazokarabati uwanja wa Shule ya msingi ya Ronald Ngala ili kuiweka kwenye hadhi bora.