Mbunge wa Taveta Naomi Shaban katika hafla ya awali. [Picha/ the-star.co.ke]

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa Taveta Naomi Shaban amepinga vikali pendekezo la baadhi ya viongozi wa Pwani ya kutaka eneo hilo kujitenga kutoka Kenya.Shaban amesema juhudi hizo zinazoongozwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi, hazina nia nzuri kwa wakaazi wa Pwani.Mbunge huyo amesema viongozi wanaodai kuwa Pwani sio Kenya walichaguliwa kupitia sheria za Kenya na kuwataka kuacha viti vya kisiasa wanavyokalia kwa sasa, kabla ya kuanza mikakati hiyo ya kujisimamia.Shaban amesema kuwa mipangilio hiyo haina maana yoyote na kuongeza kwamba inalenga kurudisha eneo la Pwani nyuma kimaendeleo."Ni jambo la kusikitisha kwamba Gavana Kingi ambaye ni wakili anaweza kufanya jambo kama hili. Nilikua natarajia kuwa atawaelimisha wenzake kuhusu sheria na kuwaeleza kuwa wamechaguliwa kupitia katiba ya Kenya basi wao ni Wakenya wanaotakiwa kujumuika kimaendeleo na wenzao," alisema Shaban.Shaban amewataka wakaazi wa Pwani kupinga wazo hilo alilosema kuwa litawaletea umaskini zaidi.Aidha, alisema kuwa eneo hilo haliwezi kujitegemea, na kuongeza kwamba matatizo yanayowakabili wakaazi wa Pwani kamwe hayawezi kutatuliwa kwa kujitenga.Shaban aliyasema haya siku ya Jumatatu alipokuwa akiwahutubia wanahabari nje ya jengo la Mahakama kuu ya Voi, baada ya kuhudhuria vikao vya kesi inayopinga ushindi wake katika uchaguzi wa Agosti 8.Kesi hiyo iliwasilishwa na aliyekuwa mpinzani wake Moris Mutiso wa chama cha ODM.Mutiso anadai kuwa Shaban alitumia mbinu zisizofaa kupata ushindi katika uchaguzi huo.Shaban aliibuka mshindi baada ya kupata kura 11,322 dhidi ya kura 11,135 alizopata Mutosi.Hata hivyo, Shaban kupitia wakili wake Noah Nyakundi aliitaka mahakama kutupilia mbali kesi hiyo huku akisema haikuwa na misingi yoyote.Mahakama inatarajiwa kuamua iwapo kesi hiyo itatupiliwa mbali au la katika kikao cha Novemba 16, 2017.