Viongozi wa Kaunti ya Mombasa wamesema kuwa wamefurahishwa na jinsi serikali ya kaunti hiyo inavyoongozwa na Gavana Hassan Joho.

Share news tips with us here at Hivisasa

Walipongeza jinsi serikali ya kaunti inavyoendesha shughuli za kaunti haswa baada ya kaunti hiyo kutotajwa kwa baadhi za zile kaunti zinazoongoza kwa ufisadi.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumanne, Mbunge wa eneo la Kisauni Rashid Bedzimba alisema kuwa licha ya misuko suko yote inayoikumba kaunti hiyo, angalau wamepata habari kuwa fedha na rasilimali za kaunti hiyo zinatumiwa vizuri.

Kauli ya mbunge huyo inajiri baada ya Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC, kutoa ripoti iliyo orodhesha kaunti fisadi mno huku kaunti ya Murang’a ikiwa ya kwanza ikifuatiliwa na kaunti ya Embu, Bomet, Kisii na Kwale.

"Kwa kaunti zote 47, Mombasa tunakabiliana na ufisadi vilivyo. Viongozi wote wanapaswa kumuunga mkono Gavana Joho katika vita dhidi ya ufisadi,” alisema Bedzimba.