Mbunge wa eneo la Mugirango Magharibi, Kaunti ya Nyamira James Gesami, ameahidi kuwa atashirikiana na serikali kuakikisha kuwa shughuli zote za mazishi ya wanafunzi kutoka Kaunti hiyo waliouawa Garissa yameshughulikiwa kikamilifu.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Haya  yanajiri baada ya familia ya mzee Onyacha, kutoka kijiji cha Engoto lokesheni ya Sironga, kupokezwa habari kuwa mwanao kwa jina Josphine Onyacha aliuawa kwenye shambulizi la kigaidi lililotekelezwa siku ya alhamisi wiki jana katika chuo kikuu cha Garissa.

Akiongea siku ya Jumatatu na wanahabari katika mji wa Nyamira, Gesami  alisema  atajaribu  kila awezalo kusaidia familia zile zilizokumbwa na mauti hayo, huku akishirikiana na serikali ya kaunti hiyo.

Familia hiyo ya Onyacha imesema wamekuwa wakimsomesha mwanao kwa hali ya umaskini, na marehemu alikuwa tegemeo katika familia hiyo, lakini kwa bahati mbaya aliuawa kwenye shambulizi hilo la Kigaidi.

“Kufariki kwa dadangu ni pigo kubwa sana, tumeshuhudia katika familia yetu  na alikwa dada aliyekuwa mtulivu kwa lolote anapoambiwa katika famila yetu,” alisema Olfha, dadake marehemu.

Wanakijiji cha Engoto wameiomba serikali ya kaunti ya Nyamira kuwasaidia katika sherehe ya mazishi, na hata chochote katika familia hiyo.