Aliyekuwa mbunge wa Nyakach, Ochieng Daima, ametishia kuelekea mahakamani iwapo zoezi la kuwasajili makurutu watakao jiunga na idara ya polisi, halitaendeshwa kwa njia huru na wazi kote nchini.
Zoezi hilo ambalo litasaidia kuongeza idadi ya maafisa wa polisi nchini limepangiwa kufanyika Aprili 20 kote nchini.
Kwenye kikao na wanahabari jijini Kisumu mnamo Alhamisi, Ochieng aliitaka serikali kuweka mikakati itakayo hakikisha kuwa zoezi hilo linafanywa kwa kufuata misingi ya katiba.
Mbunge huyo wa zamani aliwataka wale watakaosimamia zoezi la kuwasajili makurutu, kuhakikisha kuwa makurutu watakaoteuliwa kujiunga na kikosi cha polisi ni wale ambao wamehitimu.
“Wakati huu hatutakua na lingine ila kuelekea mahakamani, ikiwa zoezi hilo halitafanyika vile tunatarajia,” alisema Ochieng.
Alisema idadi kubwa ya vijana waliohitimu kimasomo wamesalia nyumbani kutokana na ufisadi, ambao umekita mizizi humu nchini na hivyo basi kulemaza juhudi za maendeleo.
Mwaka uliopita, mahakama kuu ya Nairobi ilifutilia mbali zoezi la usajili wa makurutu kufuatia madai kuwa zoezi hilo lilizongwa na visa vya ufisadi.
Hivi maajuzi Rais Uhuru Kenyatta alisema kuwa shambulizi la kigaidi katika chuo kikuu cha Garissa, lililosababisha vifo vya wanafunzi 148, lilitokea kwa sababu ya upungufu wa maafisa wa polisi nchini.