Mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung'aro amesema kuwa wakati wa viongozi kutoka kanda ya Pwani kuandaa kikao na Rais Uhuru Kenyatta ili kujadili shida zinazoikumba eneo hilo umewadia.
Akiongea katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Mungaro alisema kuwa baadhi ya viongozi nchini walikuwa wamejitokeza na kuwasilisha malalamishi ya wakaazi wao kwa rais na kupata ufadhili.
“Juzi viongozi kutoka Meru walipewa ufadhili wa kukuza zao la miraa, kisha viongozi kutoka Ukambani wakaanda kikao na rais. Mbona sisi tuachwe nyuma?” aliuliza Mung'aro.
Aidha, mbunge huyo ambaye alisema kuwa Rais Kenyatta ni rafiki wake wa karibu aliapa kuwasilisha ombi kwa niaba ya viongozi kutoka Pwani ili kuandaa kikao na rais.