Mbunge wa Malindi Willy Mtengo amewata wadau katika sekta ya kilimo kuwahamasisha wakaazi wa Pwani kuhusu mimea inayostahimili msimu wa kiangazi.
Mtengo alisema kuwa hatua hiyo itahakikisha kuwa wakaazi wanapata chakula cha kutosha hata wakati wa ukame.
Akizungumza na waandishi wa habari katika afisi yake, Mtengo alisema ipo haja ya taasisi mbalimbali za kilimo katika eneo la Pwani kushirikiana na mashirika mbalimbali ya msaada kuanzisha mafunzo hayo.
Alisema baa la njaa linaloendelea kushuhudiwa katika eneo hilo limechangiwa na hatua ya wakulima kupanda mahindi pekee wakati wa upanzi.
“Ningependa kuhimiza Kaunti za Pwani kushirikiana kwa pamoja kuanza miradi ya kutoa msaada wa chakula na maji kwa wakaazi kwani hali inazidi kuwa ngumu kila uchao,” alisema Mtengo.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya Kamshina wa Kilifi Joseph Keter kuyataja maeneo ya Ganze na Magarini kama maeneo yaliyoathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali ya kiangazi.