Mbunge wa Mvita Abdulswammad Nassir ametangaza kujitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania kiti cha ugavana katika Kaunti ya Mombasa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Nassir amesema kwa sasa anajikita zaidi katika kuwatumikia wananchi wa Mvita na kuwa atatetea kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2017.
Akizungumza katika chuo cha mafunzo ya matibabu cha KMTC tawi la Mombasa, Nassir alisema kuwa rekodi yake ya maendeleo kwa wananchi na sera zake ndio itaamua hatma yake.
“Nataka niwaambie kuwa nitarudi mwaka 2017 kuuliza kura kutoka kwa wana Mvita katika kiti hichi, na mwaka 2022 ikifika nitarudi nikibisha nyumba hadi nyumba kutaka ushirikiano wenu wa kuwa gavana wa mji huu,” alisema Nassir.
Kauli ya mbunge huyo inajiri huku gavana wa sasa HassanJoho akipigiwa upatu wa kurudi tena katika awamu ya pili ya uongozi na kisha kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.