Wenyeji wa eneo bunge la Nyaribari Masaba, Kaunti ya Kisii wamepokea kitita kikubwa cha hela za CDF zitakazotumika kukamilisha miradi ya maji na afya.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akitembelea miradi katika eneo bunge lake, mbunge wa eneo hilo, Elijah Moindi allipeana kwa mashule ya eneo hilo tanki 10 za maji za kiwango cha lita elfu kumi kila moja, pamoja na shillingi elfu hamsini za kujenga mahala pa kuwekwa tanki hizo.

Moindi alisema kuwa tanki hizo zitatumika kukusanya maji wakati wa mvua na kutumiwa na wanafunzi pamoja na wenyeji wa eneo hilo ambao wamekuwa wakitembea safari ndefu kutafuta maji.

Katika sekta ya afya, Moindi alipeana hundi za shillingi millioni mbili.

Fedha hizo zimekusudiwa kutumika katika ujenzi wa zahanati pamoja na makao ya wauguzi watakaohudumu katika zahanati hizo.

Zahanati zilizofaidika na msaada huo ni zile za Kiamokama na Ikorongo.

Mbunge huyo pia alichukua muda wake kuwahimiza wakaazi wa eneo hilo kushughulikia kikamilifu maswala ya ujenzi wa taifa na maendeleo kwani tatizo la usalama ambalo limewakumba hapo awali lilikuwa limesuluhishwa.