Mbunge wa Kinango amewataka viongozi wa mrengo wa Cord kuleta maendeleo katika eneo la Pwani.
Gonzi Rai amewakashifu viongozi wa upinzani kwa kutofanya miradi ya maendeleo eneo la Pwani, na badala yake kushinda wakilumbana na serikali ya Jubilee.
Gonzi alisema kuwa viongozi wengi wa eneo la Pwani hawafanyi miradi ya manufaa ilhali wao huwa mstari wa mbele kukashifu uongozi wa Jubilee.
“Ningependa kuwahimiza viongozi wa upinzani kukoma kuikashifu serikali ya Jubilee, na badala yake kujibiidiisha kufanya maaendeleo katika eneo hili,” alisema Gonzi.
Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa vugu vugu la wafuasi wa chama kipya cha Jubilee katika ukumbi wa Shule ya msingi ya Star of the Sea, Gonzi alisema mrengo wa upinzani wa Cord hauna ajenda zozote za maendeleo kwa Wapwani.
“Cord haina ajenda zozote za maendeleo. Kazi yao ni kelele kila siku,” alisema Gonzi.
Mbunge huyo alisema kuwa Wapwani wanahitaji maendeleo, na kuongeza kuwa mrengo wa Jubilee peke yake ndio utakaoleta maendeleo hayo.
Aidha, amewarai Wapwani kuunga mkono serikali ya Jubilee katika azma yao ya kurudi mamlakani katika uchaguzi mkuu ujao.