Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amewakashifu vikali wawakilishi wa wadi katika bunge la Kaunti ya Mombasa kwa madai ya kutumiwa na serikali ya kaunti hiyo katika kupitisha miswaada ambayo haina manufaa kwa mwananchi wa kawaida.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza katika hafla ya kuzindua rasmi kaunti ndogo ya Nyali Siku ya Jumanne, katika uwanja wa maonyesho ya Mombasa, mbunge huyo alisema kuwa kukosekana kwa upinzani katika bunge hilo kumechangia pakubwa kupitishwa kwa miswada hiyo.

“Wabunge wote ambao wako kwenye bunge la kaunti walitumia mrengo wa Cord kuingia uongozini hivyo hawawezi kumpinga Gavana Joho,” alisema Awiti.

Mbunge huyo alisema kuwa kupitishwa kwa mswada wa kuanzisha mradi wa ujenzi wa nyumba utakaogharimu serikali ya Kaunti ya Mombasa zaidi ya bilioni 200 ni mojawapo ya miswada ambayo wananchi hawakuhusishwa.

Awiti alisema kuwa ataendelea kumkosoa Gavana Joho hadi wakati ambao uongozi wa kaunti utawahusisha wakaazi wa Mombasa katika uamuzi wa miradi ambayo inatekelezwa katika kaunti hiyo.