Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir amekashifu kile alichokitaja kama kutowajibika kwa polisi katika utenda kazi wao.
Akiongea katika warsha iliyoandaliwa siku ya Jumapili ya kutamatisha mwezi mtukufu wa Ramadhan, Nassir alielezea kusikitishwa kwake na ongezeko la visa vya uhalifu.
"Watu wetu watakinai maneno yetu ya kila siku. Siku moja kutakucha na wachoke kabisa kwa kutowajibika kwetu. Nimeshindwa mimi binafsi na hali ya usalama ambayo inaendelea kuzorota kila kuchao,” alisema Nassir.
"Kama ningekuwa msimamizi wa idara ya usalama, ningeona aibu sana na kujiuzulu mara moja,” aliongeza Nassir.
Aidha, mbunge huyo aliwatuhumu polisi kwa kuwashika watu kiholela holela pasi msingi wowote.
"Polisi hapa Mombasa hawana taaluma hata kidogo kwa vile wanafanya kazi kikoloni, njia ambayo sio mwafaka,” alisema Nassir.