Wasimamizi wa shule katika eneo bunge la Bobasi kaunti ya Kisii wameombwa kuwajibika na kazi ya kusimamia shule ili kuinua viwango vya masomo katika shule wanozosimamia.
Akiongea katika hafla ya machango wa kusaidia shule ya upili ya wavulana ya Nyamache, mbunge wa Bobasi Stephen Manoti aliwaomba wasimamizi hao na kusema kuwa ni wajibu wao kuona kuwa viwango vya masomo vimenanawiri.
“Naomba wasimamizi wa shule zote za eneo hili kuhakikisha kuwa wanawajibika kazini kwani wazazi wamewachagua ili kuwawakilisha na kuongoza shule kimasomo, bali si kuleta fitina katika shule,” alihoji Manoti.
Aidha, aliwaomba wazazi kushirikiana na walimu ili kuinua viwango vya masomo, huku akitaja kuwa masomo lazima yawe na sehemu tatu ambazo ni wazazi, walimu na wanafunzi.
Aliongeza kusema kuwa sehemu moja isipowajibika, viwango vya masomo huwa vinaadhirika pakubwa, kwa hivyo ni wajibu wa wasimamizi wa shule kuleta sehemu hizo tatu pamoja kila wakati ili masomo yaweze kuendelea.
Manoti aliwaomba wanao azma ya kugombea viti katika uchaguzi ujao kusaidia shule kwanza kabla ya kuanza ‘kupiga kelele’ katika mikutano ambayo si ya kuleta maendeleo.
“Wale wanao azma ya kuwania viti katika mwaka 2017 wanastahili kuwa mahali kama hapa ili wasaidie kwanza kabla ya makelele yao,” alihoji Manoti,
Kwa upande wa msako wa pombe haramu unaoendelea, mbunge huyo aliunga serikali kuu mkono na kuwaomba watu kushirikiana na machifu wa eneo bunge ili kuhakikisha kuwa pombe haramu imeisha katika eneo bunge hilo.