Mbunge wa Nyali Hezron Awiti ametoa onyo kali kwa mabwanyenye waliohusika katika unyakuzi wa ardhi ya Soko la Kongowea.

Share news tips with us here at Hivisasa

Awiti amesema kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ili kuhakikisha kuwa ardhi hiyo imerejeshwa kwa umma.

Akizungumza siku ya Jumatano baada ya ziara ya kukagua ujenzi unaoendelea katika soko hilo, Awiti alisema kuwa zaidi ya ekari 10 katika eneo la fisheries na kipande kingine cha ardhi katika eneo la kuegesha magari zilikuwa zimenyakuliwa.

Ujenzi wa jengo hilo la kisasa umefadhiliwa na serikali kuu ikishirikiana na serikali ya Kaunti ya Mombasa.

Jengo hilo litawafaidi zaidi ya wafanyabiashara 10,000 na inakadiriwa kufungilwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta mwezi Agosti.

Wakati huo huo, mbunge huyo alisema kuwa anaunga mkono juhudi za maafisa wa polisi za kuhakikisha kuwa kundi la wahalifu la Wakali Kwanza limemalizwa.

Aidha, aliwataka viongozi wa kisiasa kutoingilia kazi ya polisi wanapokabiliana na wahalifu.

Kundi hilo limekuwa likiwahangaisha wakaazi wa Kisauni na Nyali na hata kuwadhulumu wanawake kutoka maeneo hayo kimapenzi.