Mbunge wa Kuresoi Kusini Zakayo Cheruiyot amewarai wahudumu wa Bodoboda katika eneo bunge lake kuachana na tabia ya kushiriki uhalifu ama kukodisha pikipiki zao kwa wahailifu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Cheruiyot amesema kuwa inasikitisha kuona wahudumu wa bodaboda wakitumika kufanikisha ujambazi au kushiriki ujambazi kwa kutumia pikipiki wanazomiliki.

Akiongea alipowakabidhi hundi ya shilingi elfu mia moja waendesha bodaboda katika wadi ya Mosop, Cheruiyot aliwataka wahudumu hao kuwatambua wahalifu miongoni mwao na kuwaripoti kwa polisi.

“Kuna visa vingi hapa ambapo abiria wameporwa na wahudumu wa bodaboda na wengine wanapeana bodaboda zao kwa wahalifu kwenda kuiba. Hii tabia ni lazima ikome kwa sababu nyinyi mnawajua wanaofanya hayo na ni lazima muwafichue ili wakamatwe na kufunguliwa mashtaka,” alisema.

Cheruiyot alitoa wito kwa waendesha bodaboda kuwa mstari wa mbele kudumisha usalama na kupambana na visa vya uhalifu haswa katika maeneo wanayohudumu ili kuboresha biashara yao.

“Kama watu wataendelea kuporwa wakiwa kwa bodaboda basi mtakosa biashara na ni jukumu lenu kuhakikisha kuwa kuna usalama katika steji na barabara mnazohudumu ili kuwapa abiria moyo wa kusafiri na bodaboda zenu," aliongeza.

Aidha, mbunge huyo aliwataka vijana wanaoendesha bodaboda kujiepusha na matumizi ya pombe na dawa za kulevya ikiwa wanataka kuishi maisha marefu.

“Kama utajiweka kwa kunywa pombe kila wakati na kula vitu vingene vya kuharibu mwili basi jua maisha yako yatakuwa mafupi sana ,” alionya Cheruiyot.