Mbunge wa Jomvu Badi Twalib amempa bwanyenye mmoja makataa ya siku saba kusitisha ujenzi katika kipande cha ardhi ya umma eneo la Scout, huko Miritini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Twalib alidai kuwa bwanyenye huyo amenyakua hekari kumi za ardhi hiyo yenye hekari 16.

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa, mbunge huyo alisema sharti tajiri huyo asitishe ujenzi huo au achukuliwe hatua za kisheria.

Twalib alilalamikia ongezeko la visa vya unyakuzi wa ardhi katika Kaunti ya Mombasa na ukanda wa Pwani kwa jumla, na kuitaka Tume ya ardhi nchini NLC, kutolifumbia macho swala hilo.

“Tabia hii ya kunyakua ardhi inapaswa kusitishwa mara moja kwa kuwa imepelekea wakaazi wengi kuishi maisha duni na ya uskwota,” alisema Twalib.

Aidha, aliongeza kuwa imebainika kwamba kuna baadhi ya viongozi wanaoshirikiana na mabwenyenye hao katika unyakuzi wa ardhi za umma, hatua aliyoitaja kama unyanyasaji na dhulma miongoni mwa wananchi.

Alisema kuwa hatoruhusu kamwe visa kama hivyo kuendelezwa, huku akiongeza kuwa atakayepatikana na hatia atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Vile vile, amewataka viongozi kushirikiana katika kukabiliana na swala hilo tata la ardhi, na kuwahimiza wananchi kuripoti visa kama hivyo wanapovishuhudia.