Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharif Nassir amesema kuwa amefurahishwa na juhudi za makundi ya vijana na akina mama Mombasa za kuanzisha miradi ya maendeleo.

Alisema kuwa miradi hiyo imefanikishwa kupitia kwa hazina ya Uwezo Fund iliyosambazwa kwa maeneo bunge yote nchini, kusaidia vijana na akina mama kuanzisha miradi ya maendeleo.

Akiongea baada ya kuzuru miradi hiyo siku ya Jumatatu, Nassir aliyahimiza makundi hayo kutia bidii zaidi katika miradi yao huku akiongeza kuwa juhudi zao ni ishara kwamba mabadiliko yameanza kuonekana.

“Nimefurahi kuona wananchi wakijipatia kipato kupitia jasho lao na ningependa kuhimiza vijana kutia bidii zaidi,” alisema Nassir.

Mbunge huyo alipata fursa ya kutangamana na makundi hayo na kutathmini miradi wanayoendeleza huku pia akipokea changamoto wanazopitia.

Wakati huo huo, mbunge huyo alitoa wito kwa vijana, akina mama pamoja na walemavu kuandikisha makundi yao ili kupata fedha hizo na kuanzisha miradi.

Miongoni mwa makundi yanayoendeleza miradi katika Kaunti ya Mombasa ni pamoja na Savanna Youth Group, kikundi cha akina mama cha Mwamko wa Wanawake miongoni mwa makundi mengine.

Mradi wa hazina ya Uwezo Fund ulizinduliwa rasmi mwezi Septemba mwaka 2013 na Rais Uhuru Kenyatta kwa lengo la kusaidia vijana na akina mama kujiendeleza.