Mbunge wa Msambweni Suleiman Dori katika hafla ya awali. [Picha/ the-star.co.ke]
Mbunge wa Msambweni Suleiman Dori amewataka wakaazi wa Kwale kutolipa ushuru kwa serikali ya Jubilee, kwa madai kuwa serikali hiyo haiko tayari kuboresha maisha ya Wakenya.Akiwahutubia wanahabari katika eneo bunge la Msambweni, Dori ameilaumu Jubilee kwa kupandisha gharama ya maisha hasa kwa walalahoi ambao ndio idadi kubwa ya Wakenya.“Maskini ndio wengi na wanaumia zaidi ikizingatiwa wanalipa ushuru kwa serikali,” alisema Dori.Mbunge huyo alidai kuwa serikali imewatenga wakaazi wa Kwale licha ya wao kulipa ushuru.Dori ameitaka serikali kupunguza ushuru hasa kwa wafanyabiashara wadogo kote nchini ili waweze kujinufaisha kwa kuanzisha miradi mingine.Kauli ya Dori inajiri baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwaagiza wafanyabiashara katika soko la Kongowea kutolipa ushuru kwa serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa madai kuwa wafanyabiashara hao hawapati huduma bora kutoka kwa serikali hiyo.Dori amemshutumu Rais Kenyatta kwa matamshi yake ambayo aliyataja kama uchochezi kwa wananchi.