Mbunge wa Mbeere Kaskazini Charles Njagagua ametoa wito kwa walimu kuwahimiza viongozi wa kisiasa nchini kuhubiri amani.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge huyo amesema walimu wana jukumu la kuwatadharisha wanasiasa kujiepusha na matamshi yatakayozua uhasama wa kikabila, kutokana na visa vya matamshi ya uchochezi yanayotolewa na baadhi ya wanasiasa.

Akizungumza siku ya Jumatatu katika hafla ya kuzindua sheria za mwongozo wa utendakazi wa walimu iliyoandaliwa na tume ya TSC, mbunge huyo alisema endapo taifa litakumbwa na machafuko, basi hata walimu watashindwa kutekeleza majukumu yao kwa amani.

“Nataka niwaambie walimu wazungumze na wanasiasa wanaowawakilisha kujiepusha na matamshi yatakayoleta uhasama,” alisema Njagagua.

Kauli yake inajiri baada ya viongozi wanane wa Cord pamoja na Jubilee kutiwa mbaroni na kufunguliwa mashtaka kwa madai ya kutoa matamshi ya uchochezi.

Mbunge huyo aidha alisema kuwa bunge linafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa sekta ya elimu imetengewa fedha za kutosha, ili kuiwezesha tume ya TSC kuajiri walimu zaidi.